07/07/2025
Katika historia ya mwanadamu na hata katika maandiko matakatifu, yapo tofauti kubwa kati ya viongozi wa dini na watumishi wa kweli wa Mungu.
Tatizo kubwa linalojitokeza katika jamii zetu ni kwamba watu wengi huchanganya hawa wawili kana kwamba ni kitu kimoja. Hii ni hatari, maana si kila anayevaa vazi la kidini au kusimama madhabahuni ni mjumbe wa Mungu.
1. Viongozi wa Dini ni wa mfumo – Watumishi wa Mungu ni wa kweli ya kiroho
Viongozi wa dini mara nyingi wamejikita kwenye kulinda taasisi zao, mamlaka yao, na maslahi yao. Wanaweza hata kutumika k**a vinyago vya nguvu za kisiasa au kiuchumi. Katika Biblia, Yesu aliwakemea vikali Mafarisayo, Masadukayo na walimu wa sheria kwa unafiki na kupindisha sheria kwa manufaa yao binafsi:
"Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnafunga Ufalme wa Mbinguni mbele ya watu; ninyi wenyewe hamwingii, wala hamkubali wale wanaotaka kuingia waingie." – Mathayo 23:13
2. Watumishi wa Mungu wamesimama na Haki, hata ikiumiza
Watumishi wa Mungu, k**a manabii wa zamani – Eliya, Isaya, Yeremia, na Yohana Mbatizaji – waliikemea jamii kwa uovu wake bila kuogopa. Hawakubembeleza mamlaka wala kukubali kununuliwa. Walikuwa tayari hata kufungwa, kuteswa au kuuawa kwa ajili ya kusimamia ukweli wa Mungu. Watumishi wa namna hii ni nadra sana leo.
3. Viongozi wa Dini hutafuta makundi – Watumishi wa Mungu hutafuta nafsi za watu
Viongozi wa dini hujenga maelfu ya wafuasi lakini mioyo ya watu hubaki tupu. Wanahubiri kwa faida, wakigeuza watu kuwa chanzo cha kipato. Lakini watumishi wa Mungu hujenga watu, si majengo wala majina. Huduma yao huzaa toba, haki, na ukombozi wa kweli.
4. Hadithi za Mafarisayo na Masadukayo ni onyo la historia
Yesu Kristo hakuwahi kuwa karibu na viongozi wa dini wa wakati wake. Aliwakemea kwa unafiki wao, kwa kutumia dini k**a silaha ya kuwatesa wengine. Hili ni onyo kubwa kwa vizazi vya sasa – kwamba dini isipotenganishwa na mamlaka ya kiroho, inaweza kuwa chombo cha uonevu na utumwa mpya wa kiakili na kiroho.